Nyota ya Maulid Machaprala
Yussuf H. Kombo +255 713 459447 au 0772 371701
Zanzibar ni visiwa ambavyo hakika aliyebuni jina hili basi mungu ampe rehma. Ni jina ambalo limetokea kuwa na mvuto mkubwa katika jamii zetu na dunia nzima. Zanzibar ina mvuto wa kimaumbile ikiwemo visiwa, ina mvuto wa kihaiba, ina mvuto wa rutuba, ina mvuto wa kimazingira, ina mvuto wa kisiasa, ina mvuito wa kiuchumi, ina mvuto wa kihistoria, ina mvuto wa kimichezo na zaidi ni mvuto kwa kiutamaduni.
Utamaduni wa Zanzibar umechanganyika. Kuna ule wa Ki-Afrika bantu, kiasia, Kizungu, kichina na hata ule wa kimarekani. Upo ushahidi wa haya yote katika hisitoria za Zanzibar. Jamii ya Ki-Zanzibari ni mchanaganyiko wa watu kutoka kila pembe ya Dunia ingawa Wa-Africa ndio asilimia kubwa. Tamaduni za mila mbali mbali. Baadhi zina ushahidi wa wazi na zipo ambao zinafifia. Pia zipo ambazo waliowengi hawafahamu uasili wake.
Kwa mfano ngoma za mdundiko. Hii asili yake morogoro na uzaramoni. Ngoma ya tukulanga, hii asili yake Kigoma kwa Wamanyema, maulid ya homu asili yake arabuni (Yemen), nachi asili yake India, chakacha asili yake pwani ya mwambao wa Mombasa, Samba asili yake Ureno, mbwa kachoka au beni – asili yake ureno na spain ikiwa na asili ya samba kama ile ya Brazil na nyingi nyingine ambazo sitozitaja. Lakini mbali na ngoma tu bali hata majina ya watu pia yana asili mbali mbali mfano Mlekwa (wanyamwezi – ikiwa na maana ya mtoto aliyefiwa na mama yake mara tu baada ya kuzaliwa), Mwita (wakuraya), saliboko (wasukuma), shomari (wazaramo), hoko (wachina), gomez (waspain) nk. Mitaa pia iko hivyo hivyo na hata vyakula vya Zanzibar vina majina ya kigeni mfano kachori (kihindi), haluwa (kiarabu), slesi (kingereza), bendera kitalioana, koja (kireno/kispain) n.k
Kilichoni gusa hasa leo na kilichonifanya niandike habari hii leo ni utajiri wa Zanzibar katika fani ya muziki, hususan huu muziki wa Taarabu. Muziki huu ambao kwa sasa umedakiwa na watalaam wa kugeuza mambo waliofikia hadi kuuita ”rusha roho” umekuwa ni hazina kubwa ya sura ya Zanzibar. Lakini mimi leo sina la kuogelea katika rusha roho wa rusha gondi, ila nimenaswa na asilia. Hasa muziki laini unaogusa nyoyo za watu wasio na na roho tembe. Watu wenye uono na uchambuzi wasiopenda kupambanua mambo makubwa utuni.
Muziki wa tarabu asili una msisimko na mara chache sana huwa na mhemko. Mtu aweza kula akiwa kitini ananesa. Anaweza kucheka akiwa kitini anayumba na anaweza kununa akiwa kaa na kuongea kwa macho na ishara. Hii hi ni taarabu ya ishara.
Katika fani hii wapo wengi walio bobea. Wapo wapiga ala za muziki, wapo watunzi na wapo waimbaji. Waimbaji wapo wa kike na wa kiume. Siwamalizi kuwataja lakini leo hamu yangu ni kumtaja mmoja wao nae ni Maulid Machaprala. Ah, Mungu amlaze pema, Mungu ampe nusura huko aliko. Huyu naweza kumuita Muimbaji wa karne katika waimbaji wanaume hapa Zanzibar. Wakishindanishwa na Bakari Abeid, sijui nani atashinda lakini mimi kura yangu nampa yeye. Gwiji hili limeimba nyimbo nyingi, lakini mimi nisikiapo nyota na niulamu moyo au macho huwa sina nguvu kabisa na baadhi ya wakati hutokwa na machozi. Hasa hii nyota.
Basi leo naomba niuchambue huu wimbo nyota NYOTA ulioimbwa Maulidi Machaprala ambae naweza kusema kwa karne ya ishini na ishirini na moja anaweza kuwa katika watatu bora kwa waimbaji wanaume. Kuna kila sababu ya kusema hivyo kwa Maulid Machaprala. Wimbo huu nyota beti zake zinasomeka kama ifuatavyo:
Nyota nakuamini, dira na ramani
Nimo safarini, siwasili pwani
Wasemao siponi, wasisibu ya Manani
Nyota tokea zamani, naelewa na sukani
Siibaini sioni, ikowapi pwani pwani
Huu leo mtihani, nasubiri yake shani
Dhoruba na matufani, zivumazo baharini
Nyota tena sizioni, nahiliki mawimbini
Sioni sionekani, nimefunikwa kizani
Bandari nitaegesha, nipokewe kwa bashasha
Rabi taniwasilisha, na hatari kunivusha
Anivue vya kutisha, na salama kunivesha
Katika wimbo huu Maulid anasema na yota. Maulid analia na nyota, Maulid anasikitika na nyota. Nyota katika wimbo huu inampa Machaprala hisia kali za huzuni ambazo bila shaka alipatwa na hisia za kutengana na mpenzi wake wakati alipopatwa na mashahibu mabaya yakiwemo maradhi na maummivu ya khuba.
Penzi lake ambalo alilielekeza kwa mpezi wake hapa limechimbuliwa kama ni safari na hadi atakapolipata kwa nafasi basi kuna maswahibu yatampata njiani. Bila shaka penzi lake lilikuwa na waliokuwa wakilikodolea macho na hawa walitamani amalizike nawo washike nafasi. Walimuombea mengi yakiwemo mauti lakini Maulid aliyafahamu hayo na ndipo akamuomba mola asiwatakabalie maombi yao.
Machaprala alimuamini sana mpenzi wake kiasi cha kufuata na kutekeleza aliyoshauriwa. Kwake yeye haya yalikuwa ni kama dira na ramani ya maisha yake. Haya yamo katika beti ya kwanza ya wimbo huu NYOTA na ubeti huo unasomeka hivi.
Nyota nakuamini, dira na ramani
Nimo safarini, siwasili pwani
Wasemao siponi, wasisibu ya Manani
Katika jahazi hapo zamani na hadi sasa manahodha hutumia nyota kutunga shabaha ya kule waendako na kupata muwelekeo majini. Ni nyota zilizowaongoza hadi kufika safari zao. Bila shaka wakati nahodha anasoma nyota ili kupata muwelekeo bila shaka usukani nao ulikuwa na jukumu la kuongoza chombo kuelekea kunakotakiwa kwa kufuata miongozo ya nyota. Kwa mantinki hii ndipo manahodha walipofanikiwa kuwa manahodha wazuri tangu zamani.
Machaprala amemithilisha penzi lake, imani na uwerevu wa mpenzi wake na mfumo wa uendeshaji wa jahazi, kwamba nyota ndio kiongozi. Amekiri kuwa upeo wake wa kuona umefifia haoni na alikuwa anatafuta wapi ilipo pwani akiwa bahari kuu. Alitaka kutua apumzike na apate faraja lakini hakuwa na hila na alikabiliwa na mtihani. Kilichosalia ni rehema za Mungu ambazo kwake amezitaja kama shani. Si wengi walio na moyo wa Machaprala wa kuelewa haki na uwezo wa nyota katika kuiongoza sukani. Lakini kukiri udhaifu pia ni jambo kubwa ambalo chozi lake ni dhahabu kwa anaeliliwa iwapo anajua chozi la raha na ghuba linavyounguza. Ubeti huu wa pili unawasilisha hisia kama ifuatavyo:
Nyota tokea zamani, naelewa na sukani
Siibaini sioni, ikowapi pwani pwani
Huu leo mtihani, nasubiri yake shani
Mbali na kuuachia moyo wake kwa aliyempenda, lakini haikuwa dawa. Bado aliandamwa na mafisadi. Walifisidi penzi lake kiasi cha kupoteza hadhi yake na ladha yake. Kwake hii ilikuwa ni hilaki kubwa na ilimfanya awe baidi na kimya kiasi ya kutokadiriwa mema. Ujusuri moyoni haukwisha ingawa alichoka. Kama wapo ambao huwa wanakata tamaa wapatapo idhilali, basi Machaprala hilo alikuwa akilichelea ingawa alikiri kuwa alikuwa katika wakati mgumu. Maulid anasema.
Dhoruba na matufani, zivumazo baharini
Nyota tena sizioni, nahiliki mawimbini
Sioni sionekani, nimefunikwa kizani
Pia aliamini kuwa ingawa yupweke katika vita vya nafsi na watu, lakini alikuwa na tamaa atashinda na atafanikwa siku ikifika. Hapa anajipa moyo.
Bandari nitaegesha, nipokewe kwa bashasha
Rabi taniwasilisha, na hatari kunivusha
Anivue vya kutisha, na salama kunivesha
Ndugu wasomaji nimendika makala haya mbali na kutoa uchambuzi na watu kufahamu undani wa nyimbo hii, nimeguswa sana na maonesho ya Zanzibar. Si mengine bali ni tamasha la nchi ya jahazi. Usukani, Bahari, mawinbi, upepo, nyota na dhoruba ni vitu vyenye uhusiano mkubwa na jahazi. Maulid machaprala amevigusa vyote hivyo katika nyimbo hii. Sifahamu kama alijua siku moja kutakuwa na tamasha la jahazi ambao wimbo wake umegusa baadhi ya maeneo. Wimbo huu unaivusha Zanziar kiutalii na hasa pale utakapofafanuliwa zaidi kama hivi. Ni matumaini yangu kuwa utapata muda wa kuusikiliza tena leo la nakuomba msikilize Maulid Machaprala anavyonung’unika na kusononeka.
Je wako wapi wajifanyao werevu wa mambo?. Tuchambulieni tuone, fafanueni tufahamu,
Mungu mlaze mahala pema peponio – AMIN
Yussuf H. Kombo MSc. (THE HERBALIST OF ZANZIBAR)
Emails: yussuf.kombo@hotmail,
yhkombo@yahoo.com
Mobile: +255 713 4594, +255 772 371701
Pia Nisome katika mtandao:
http://komboherb.blogspot.com
No comments:
Post a Comment